Watu wengi katika dunia ya leo wameshindwa kufanikiwa ama kufikia malengo na ndoto zao kwa sababu ya hofu yakufanya kile ambacho wao huweza kuwatimizia malengo yao. Na hofu hiyoimewakosesha amani, ujasiri, na kutokujiamini juu ya masuala wanayoyahitaji katikashughuli zao kwa namna moja ama nyingine. Hofu inapotawala sana hutengeneza
kushindwa. Ukiishi ndani ya msukumo wa hofu kila hatua moja utakayopiga kwenda
mbele, hofu itakurudisha hatua moja au zaidi nyuma.
Miaka ya 2007 kwenda 2008,
nilikuwa napenda sana kuitazama mieleka. Mieleka ni mchezo hatari sana
unaopendwa hasa na watu wa ughaibuni, ndio maana wanatoa onyo kali ya kwamba
usijaribu mchezo huo, kwa sababu ni mchezo usio na utofauti na vita. Katika
mieleka watu huweza kuumia vibaya, kupata ulemavu wa kudumu hata kupelekea
kifo. Japo kuwa kuna hatari katika mchezo huo, watu wamekua wakiendelea
kuucheza na wengine kujiunga kuucheza, ingawa onyo kali limetolewa. Kitu
nilichojifunza kutoka kwa washiriki wa mchezo huo ujasiri wa kutafuta pesa na
mafanikio. Kitu kingine ni nini hasa kinachowafanya waendelee kuucheza na
kujiunga kushiriki mchezo huo, ni kwa sababu wamekubali kuiondoa hofu ndani yao
juu ya mchezo huo hatari.
Wacheza mieleka wanaamini ikiwa utakuwa na hofu hautaweza
kushiriki katika mchezo huo na wala hautaweza kupata mafanikio. Swali la
kujiuliza kama watu wameondoa hofu zao juu ya mchezo huo hatari, kwanini hofu
ikuzuie wewe kufanya kile unachotaka kukifanya ili kutimiza ndoto zako?
Hofu ni zile hisia za ndani kabisa ambazo hutujaza hali ya wasiwasi, mashaka,
mfadhaiko, woga au utisho juu ya jambo Fulani. Hofu ni matokea ya mtu kujiona
huwezi, haujikubali na hauna uhakika wa mambo unayoyafanya. Kitu
kinawatofautisha watu waliofanikiwa na wasiofanikiwa ni namna ya kukabiliana na
hofu.
Duniani kote hakuna mtu aliyeweza kufanikiwa kwa kuogopa hofu, iwapo mtu akishindwa
kuhimili kuishinda hofu basi hatoweza kufanikiwa.
Yatupasa kufahamu kuwa hofu hutengenezwa na mazingira uliyonayo au unayoishi,
na baadae huingia ndani ya mtu taratibu kisha kukua hadi kukomaa. Hofu ikikomaa
ni hatari zaidi. Hofu sio kitu halisi cha kuhofia, watu wamekua wakihofia hofu
bila kuifahamu hofu ikoje. Kama nilivyosema hapo awali kuwa hofu hujazwa na
kutokujiamini, kujikubali, kuogopa kutenda jambo Fulani. Hofu ni picha tu,
inayomtokea mtu anapotaka kutenda japo Fulani kwa mfano. Unataka kuwa mwandishi
wa vitabu, inakujia picha (hofu) kwa uwezo wako huu mdogo ni nani atapoteza
muda wake kusoma vitabu vyako? Je utawezaje kuwachukua wasomaji na kuwavutia
kusoma vitabu vyako wakati wamezoea kusoma vitabu vya waandishi Fulani
mashuhuri? Una kitu gani kipya cha kukiandika na kuwaambia watu wakati kila
kitu kimeshasemwa na waandishi wengine waliopita na waliopo?
Hiyo ndiyo hofu
hujengeka kutokana na hali ya kutokujiamini na kukithamini kile ulichonacho.
Kuna muda unahitaji kufanya kilimo, biashara au shughuli yoyote ile ya maslahi
kwako ila hofu inakuzuia. Ikiwa utaruhusu hofu kukuingia na ukaikubali,
hautaweza kuifanya shughuli hiyo na kuifanikisha. Hofu itakutengenezea picha ya
kuona hasara peke yake juu ya jambo unalotaka kulifanya.
Fahamu kuwa tabia ya
hofu kwa kiasi kikubwa ni kutoa matokeo hasi.
Wakati mwingine hofu inatengenezwa toka tukiwa watoto au katika mazingira
tunayokulia. Hofu hizi zinajengwa na kukuzwa katika akili yetu na ndizo huleta
madhara.
Kwa mfano, watoto wengi wamasikini wamejengewa hofu ya kutojaribu au kufanya
shughuli zitakazo wapa mafanikio kwa kuambiwa maneno ya kukatisha tamaa kama
"maji hufuata mkondo" ikimaanisha kama wewe ni maskini utakufa
maskini, kwa sababu utaishi maisha ya kimaskini waliyopita wazazi wako na
ndugu. Au “unaambiwa mkono mtupu” haulambwi hii inaamisha wewe na umaskini
ambao umezaliwa ndani yake huwezi kuwa na positive impact (matokeo chanya)
katika jamii yako, isipokuwa wanaopaswa kufanya shughuli hizo na kuwa na
positive impact ni matajiri peke yao.
Pia kuna hofu imejengwa ndani yetu kuwa
mtu hawezi kufanikiwa ikiwa atatokea mazingira duni, kwa mfano shule za kata,
kutokana na mazingira yaliyopo katika shule hizo, ikiwa mtoto ataenda kusoma huko,
atakuwa ametimiza wajibu wa haki ya mtoto kupata elimu na sio kupata mafanikio.
Hofu inapojengwa hukua na kukomaa katika fikra na bongo za watoto, hivyo
huwatengenezea mazingira ya kuogopa kujaribu au kufanya mambo makubwa na yenye
maslahi kwao, kwa kuwa hofu imo ndani yao. Asilimia kubwa mazingira ya hofu
toka utotoni na mazingira unayokulia hujengwa na wazazi wetu na watu wa karibu.
Hofu pia hujengwa na mambo yaliyotokea, yanayotokea na ambayo hayajatokea.
Katika hali ya kawaida tu, ni vigumu kuiepuka hofu, kwa sababu ni changamoto
ambayo kila mmoja lazima aipitie. Unaweza ukapata hofu ya kutenda jambo fulani
kwa sababu kuna ndugu, rafiki au jamaa yoyote unaemfahamu alifanya na
hakufanikisha, alikwama, aliharibu, au alipata hasara. Kutokana na kuiona hali
hiyo mwenyewe, unaanza kupata hofu ya kutokufanya hiko kitu (shughuli) ukihofia
na wewe usije ukapata hasara kama walivyopata hasara wengine au unaweza pata
hofu ya kufanya kitu fulani (jambo) kwa kuwa hujiamini kama unaweza kukifanya
au haujawahi kukifanya.
Maisha yako ni sawa na chombo cha usafiri na dereva wake ni wewe mwenyewe, na
wala usitegemee kama kuna anaeweza kuja kuyaendesha maisha yako.
Na ikiwa
utategemea mtu mwingine ayaendeshe maisha yako, ukweli ni kwamba kuna anguko
kubwa sana linalokuja kukutokea mbele yako, kwa sababu kila mtu anajukumu la
kuyaendesha maisha yake na kama mtu akiendesha maisha yako hatayaendesha kama
maisha yako bali ataendesha kama maisha yake, na siku itakapo tokea hayupo
ndipo maisha yako yataenda mlama au kuharibika kabisa.
Uendeshaji wa chombo cha
usafiri inahitaji ujasiri wa hali ya juu ili kuweza kukiongoza chombo hicho.
Haitakiwi kuwa na hofu kwa sababu ya vitu vinavyoweza kukutokea kama uharibifu
wa chombo hiko, ajali ama vitu vingine vya kuogofya vinavyoweza kujitokeza.
Ndivyo ilivyo katika maisha halisi kuna misukosuko, kushindwa, kuumia na vitu
vingine vingi vinavyoweza kukusababishia kutoyafikia malengo yako.
Ondoa kwanza
hofu na uwe jasiri ili ukabiliane na changamoto hizo. Kama utaruhusu
kuyaendesha maisha yako ukiwa umejawa na hofu ndani yako, tayari utakuwa
umeshazuia kutimia kwa mafanikio yako. Unao uamuzi wa kuendesha maisha yako
vile uonavyo wewe inafaa, ila usikubali hofu ikuingie wakati unayaendesha
maisha yako. Hofu haishindwi kwa maneno, inahitaji kupingwa kwa utayari na na vitendo.
Imeandaliwa na;
Moses Chris Lumole
Teacher, Writer and Inspirational Speaker.
Phone: 0659230954
Email: lumolemoseschris@gmail.com©2016
No comments:
Post a Comment